Wednesday, June 29, 2011

WAZUNGU WACHACHAMAA ISHU YA RADA!

Waandamaji Majuu wakipinga uhuni waliofanyiwa Watanzania kutoka kwa BAE

Desemba mwaka jana SFO (Serious Fraud Office) Uingereza iliiamuru  kampuni ya BAE Systems inayouza vifaa vya ulinzi ulimwenguni kulipa faini kama adhabu ya shughuli zake mbovu za kibiashara na serikali za Saudi Arabia na Tanzania. Mwezi Februari 2011 BAE ilikubali sharti ambalo ni kuilipa SFO paundi milioni 285 na serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni (shilingi 75.3 bilioni), kama pesa za kujisafisha uso; ikiwa ni kuueleza ulimwengu mzima kuwa kampuni hiyo tajiri yenye wafanyakazi laki moja duniani, ina maadili mema.
Toka tamko litokee imezuka migogoro kadhaa.
Bonde moja wamesimama wananchi Bongo wasioamini viongozi  kwamba wana malengo ya kutetea maslahi yao. Hapo hapo, BAE Systems imetoa kauli kwamba pesa  ziende kwenye mashirika ya fadhila( na NGO) Tanzania ambayo kawaida ni ya kigeni. Imedaiwa barua zimeandikwa na wananchi kuiomba BAE isiipe serikali pesa hizo.
Kilima kingine wamekaa wabunge na viongozi wa serikali wanaoamini huu ni ukoloni mambo leo. Kwamba nchi tajiri kuiamuru nchi changa namna ya kufanya mambo yake ni utumiaji mabavu kiuchumi.
Kihistoria baada ya Waafrika kutawaliwa miaka zaidi ya 60 tuliachwa maskini na wale waliojali maslahi ya raia waliondolewa na Wazungu, mathalan Patrice Lumumba wa Kongo alieuawa 1961 na nafasi yake kuchukuliwa na Joseph Mobutu. Toka Jenerali Mobutu alipochukua madaraka mwaka 1965  hadi leo Kongo-Zaire imeharibiwa kabisa.
Wapo waliomudu kama Mwalimu Nyerere aliyetetea Uafrika na kujenga amani Tanzania ambayo tunayo hadi leo.
Toka habari kuhusu Wabunge wanne kuja Uingereza kuzungumzia mtafaruku huu  chuki na hasira iliyoenea kutokana na ufisadi ni kama imewashwa; kidonda kimetoneshwa. Mhusika mmojawapo wa tukio la 1999,  Shailesh Vithlani ambaye inadaiwa alipewa hongo kutimiza dili, hajulikani aliko. Hata baada ya mahakama ya Uingereza chini ya Justice Bean kuamuru ashtakiwe bado bwana Vithlani yadaiwa anajificha Uswisi.
Je, tutajuaje kwamba Wabunge wetu wanalo zuri moyoni, wanauliza wasomaji wengi mitandaoni? Je wahusika wengine katika dili hilo ambao bado wako serikalini wamefikia wapi? Je, tutaamini vipi kwamba mabilioni haya ya Waingereza yatatumiwa kusaidia elimu ya watoto wetu nchini, kama wanavyoahidi?
Hatuwezi kujua.
Tunaloweza kulifanya ni kuamini.
Kwa vipi?
Wakiongea katika Ubalozi wetu Uingereza mjini London, juma lililopita viongozi hao chini ya Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai walihimiza  kuwa wanafuatilia matokeo ya mahakama ya sheria Uingereza inayochunguza rushwa (SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo riba inaongezeka.
Kampuni ya BAE systems huuzia ulimwengu mzima silaha mbalimbali za ulinzi wa majini, ardhini na anga, pia vifaa vya kisasa  vya mawasiliano ya habari, umeme, usalama na teknolojia. Mwaka jana BAE systems ilipata faida ya paundi bilioni 22.4 (takribani shilingi trilioni 60).
Wabunge walikutana na “House of Lords” ambacho ni kitengo cha juu Bunge la Uingereza chenye usemi mzito nchi hii ya Malkia. Walikutana pia na Wabunge wenzao akiwemo Naibu Spika wa Bunge Lindsay Hoyle. Walitegemewa pia kukutana na maofisa wa kampuni ya BAE Systems Philip Bramwell na Lesley Collen.
Mbunge, John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Hesabu za Umma,  aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika kujenga elimu,” alisema mwakilishi huyu wa Bariadi Mashariki.
Wabunge walionyesha nia ya kutaka kusafisha jina la Tanzania, kurekebisha jina la viongozi wetu na kuleta sura mpya ya mambo yanayoiharibu Afrika.
Walisisitiza na kuahidi kinaga ubaga kwamba pesa zitaendeleza elimu.
Kauli yao ina maana macho yote yanawatazama na kuwategemea kama mashujaa wapya. Tusiwahukumu kabla hata ya kuanza.
Itakuwa vyema tukiikubali kauli yao kuwa wanadhamiria kutumia nafasi yao walioipatia kupitia kura za kidemokrasia kutenda la maana. Hakuna haja ya kumzomea mtu anayejaribu uzuri. Mwache kwanza amalize anachokidhamiria kabla ya kupiga kelele. La maana kwa sasa ni kuwatakia kheri maana kuna mawili. Nchi yetu kudharauliwa na wageni na  huduma mojawapo muhimu nchini, yaani elimu, kukidhiwa.
 
 Sasa hivi kweli tukibadilishana meza, tuseme Tanzania ndio tuwe na uwezo wa kufanya utapeli kwa kuwauzia rada Waingereza? Kisha  baadaye watushtukie kuwa tulifanya rafu?  Halafu sisi tuwaambie kuwa tutawalipa baadhi ya fedha kutumia NGOs zetu?  Je, tutakuwa salama? Je mnadhani Waingereza wataukubali usanii huo?
MGOGORO WA RADA ZA NDEGE BAINA SERIKALI NA BAE SYSTEM UNAWEZA KUWA CHANZO CHA UONGOZI BORA TANZANIA
Tafakari.
Asanteni,
*Imeandikwa na Freddy Macha pamoja na URBAN PULSE wakishirikiana na Jestina George

No comments:

Post a Comment