Thursday, June 23, 2011

SHIRIKA LA KIVULINI LAANDAA WAPAMBANAJI.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mbinu za uongozi jijini Mwanza.
 

KUNA DALILI kuwa tatizo la mfumo dume katika jamii sasa linaelekea kufikia kikomo na wanawake kushika hatamu ya uongozi.

Dalili hizo zinatokana na kitendo cha wasichana 41 wa jiji la Mwanza kuamua kujiwekea mikakati ya kuwa viongozi na wanaharakati kupambana na tatizo la mfumo dume katika jamii.

Wakizungumza mara baada ya kumalizika mafunzo ya mbinu za uongozi kwa wasichana “Young Women Leadership Skills” yaliyoendeshwa na Shirika la kutetea haki za Wanawake, KIVULINI mjini Mwanza walisema kuwa sasa wako tayari kupambana na wanaume katika nafasi mbalimbali za uongozi.
           
Wasichana hao walioshiriki mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyomalizika Juni 17 mwaka huu walisema kuwa mafunzo waliyopata yamewapa uwezo mkubwa wa kujiamini na kuweza kusimama mahala popote kugombea nafasi ya uongozi pindi inapotokea.

Aidha, msemo ulizoeleka katika jamii kuwa kumwelimisha mwanamke ni sawa kuelimisha taifa, ulionekana kuwa silaha kubwa inayompa ujasiri msichana wa Mwanza kuanza harakati za kutetea haki zao na kuleta mabadiliko katika jamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasichana hao walibainisha kuwa kuwepo kwa tatizo la mfumo dume katika jamii ni matokeo ya wanawake kutoandaliwa mapema kushika nafasi za juu za uongozi kwani mara zote nafasi hutokea kwa mtu aliyejiandaa vyema na si suala la bahati.
 
Mmoja wa washiriki Jasmine Jamal (15) ambaye pia ni katibu wa mabaraza ya watoto taifa na  mkoa wa Mwanza alisema kuwa mafunzo hayo yamemwongezea ushawishi wa kufikia malengo yake ambapo hakusita kueleza nia yake ya kuwania Ubunge mwaka 2020.

Jasmine anasema kuwa binafsi mafunzo yamempa mwanga ambapo sasa ameanza kuona picha kuwa mfumo dume na mila potofu zilizomkandamiza mwanawake kuwa hawezi sasa vinaelekea kufikia ukomo wake kutokana na mwamuko aliouona kutoka kwa washiriki wenzake.

Katibu huyo wa mabaraza ya watoto ambaye pia ni mshauri nasaha katika shule yake ya sekondari ya Butimba Day na mtangazaji maarufu wa Redio SAUT anaongeza kuwa mafunzo aliyopata yamezidi kumwaminisha kuwa wanawake wanaweza bila hata kuwezeshwa wakiwa na malengo yaliyo bayana.

Aidha alitoa wito kwa wasichana na watoto wenzake kutokubali kukatishwa tamaa na utamaduni uliozoeleka kuwa wanaume ndio tu wanaoweza kushika nafasi za juu za uongozi bali watumie nafasi wanazozipata kupambana kikamilifu ili kuishawishi jamii kuwaamini na kuwapa dhamana kubwa za uongozi.

Mshiriki mwingine Rehema Meshack(19) naye akiwa na ndoto za kugombea Ubunge alisema kuwa semina hiyo imekuja wakati muafaka na kuitaka serikali na vyama vya siasa kuweka mazingira mazuri ya kuwapata viongozi wanawake na kuzingatia suala la mgombea binafsi wakati wa kuandika katiba mpya.

Rehema anasema kuwa wasichana wengi wana rekodi nzuri za uongozi ambazo zinazotakiwa kuendelezwa na kuwaongezea mbinu za kufikia malengo waliyojiwekea na pia kuwajengea matumaini mapya waliokwisha kukatishwa tamaa na dhana ya mfumo dume.

“… Kwa mfano mimi nimekuwa mjumbe wa Baraza la watoto nikiwa na miaka Saba, mwaka 2006 hadi 2007 nikawa Mhasibu, mwaka 2008 Mwenyekiti wa baraza hilo mkoa wa Shinyanga ambapo mwaka huo huo hadi mwaka 2010 niliochaguliwa kuwa Mhasibu katika ngazi ya taifa” alisema Rehema.

Aliongeza kuwa baada ya kustaafu, Rehema ameendelea kuwa Mshauri wa mabaraza hayo taifa na mkoa wa Mwanza ambapo baada ya mafunzo ya mbinu za uongozi  anakusudia kuanzisha NGO yake kuwasaidia watoto na wasichana wenzake katika harakati za kuwania uongozi katika chaguzi mbalimbali.

Kwa upande wake mshiriki kutoka shule ya sekondari Mnarani, Christina Joseph (K.IV) alisema kuwa mafunzo aliyoyapata yamekuwa nguzo kuu ya kuchochea hamu yake kuwa Mwanasheria maarufu nchini.
Alisema kuwa pamoja na kujifunza aina na mbinu mbalimbali za uongozi kwa lengo la kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi za uongozi nchini amegundua pia kuwa elimu ni nyenzo kuu katika kufika malengo.

Naye Safaa Ally (26) alibainisha kuwa ili kuwa mpambanaji na kiongozi mzuri wa baadaye msichana anapaswa kwanza kuwa kiongozi wa mwili wake mwenyewe na kujijengea taswira nzuri katika jamii kwa kuepuka mimba za utotoni ambazo uwafanya wengi wao kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.

Washiriki waliongeza kuwa endapo kila mtoto ataziishi ndoto zake za kuwa mtu fulani katika jamii wanazojiwekea tangu utotoni itakuwa silaha kubwa ya kukomesha mimba za utotoni au ndoa katika umri mdogo hivyo kufika pale wanapopataka.

Kwa upande wa baadhi ya wasichana viongozi waliotoa mada katika semina hiyo, Waziri wa jinsia na mambo ya jamii ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha St. Augustine Bi.Juliana Ezekiel na makamu wa rais wa Chuo hicho Bi. Anna Mushi, pamoja na kusisitiza suala la kujiamini pia walitoa nguzo nne za kuwa kiongozi.

Wlizitaja nguzo hizo zitakazo wasaidia wanawake kupambana na mfumo dume katika jimii kuwa ni pamoja na kuwa na ndoto, kumcha Mungu, kujituma na kuhakikisha wantumia njia sahihi  kuyafikia malengo yao.

  “Wanawake wajiamini kuwa wanaweza bila hata kuwezeshwa kwani mifano ni mingi, tunawaona wamama wenzetu kama naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Spika wa Bunge la Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda, Rais wa Liberia na Mkurugenzi wa Kivulini Bi. Maimuna Kanyamala... Wanawake tuamini tunaweza!” walisema viongozi hao wa SAUT.

Juliana na Anna walishauri pia mafunzo hayo kufanyika mara kwa mara ili kuwaweka wasichana katika hali ya utayari pindi nafasi za kuongoza zinapojitokeza na kuyaomba mashirika mengine kuiga mfano wa KIVULINI.

 Naye mkufunzi katika semina hiyo Bw. Benard Makachia alisisitiza kwamba kuwa mwanaume siyo kigezo tosha cha kuwa kiongozi na kuitaka jamii kuondokana na dhana potofu kwani uongozi ni mchakato ambapo wanawake wakiandaliwa vizuri wanaweza kuongoza.

Bw. Makachia anaamini kuwa mikono inayolea mtoto ndiyo inayolea dunia na kwamba nchi zote zinazoongozwa na wanawake zinakuwa katika mikono salama akitolea mfano nchi za Liberia n.k.

 “Mfano, Tembo/ndovu nchini India pamoja maguvu waliyonayo hufungwa kwa kamba tena nyepesi lakini hawatoroki kutokana na jinsi walivyokuzwa tangu utotoni…Unapomwambia mtoto ‘acha kulia kama mwanamke..jikaze kiume..nk’ unamjengea dhana kuwa mwanamke ni mtu duni” alisema Bw. Makachia.

Akieleza malengo ya mafunzo hayo Mkurugezi mtendaji wa KIVULINI Bi.Maimuna Kanyamala alisema kuwa ni kuwaongezea ufahamu wasichana kuhusu haki za wanawake na haki za binadamu sambamba na kuwaanda kushika nafasi pindi wanawake waliopo katika ngazi za uongozi wanapostaafu.

Aidha, Bi. Maimuna aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuziba mwanya (gap) kati ya viongozi wanawake na wanaume ambapo takwimu zinaonyesha kuwepo kwa pengo kubwa kati yao.
    
 “Tunawaandaa wanawake ili kuziba pengo kwani wanawake wanaweza kuongoza tatizo ni kuchelewa kwa fursa za wao kujitambua” alisema Bi. Maimuna.

Kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA) toleo la mwaka 2009 “umasikini na maendeleo ya watu” pamoja na viti maalumu, jumla ya wabunge wanawake walikuwa 75 kati ya wabunge 323 wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia uchaguzi wa mwaka 2005.

MKUKUTA walibainisha pia ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika utumishi wa umma kutoka asilimia 20 mwaka 2005 hadi 22 mwaka 2009.

Ongezeko jingine la kupigiwa mfano ni katika nafasi za majaji kutoka majaji wanawake nane hadi 24, makatibu wa kudumu (Permanent Secretaries) saba hadi tisa na manaibu wake mmoja mpaka kufikia watatu ambapo kwa upande wa makatibu tawala wa mikoa (RAS) waliongezeka kutoka watano mpaka saba.

Kwa upande wa serikali za mitaa katika ngazi za vijiji, kata na halmashauri takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la asilimia 18.6 (2006) kutoka asilimia 9.6 mwaka 2003 wanaume wakiwa kati ya asilimia 26.6 (2006) na 24.2 mwaka 2003.

 Mafunzo ya kumjengea uwezo mwanamke kwa nia ya kukabiliana na pengo hilo yamekuwa yakiendeshwa na shirika la KIVULINI katika wilaya mbalimbali za kanda ya Ziwa na mkoani Singida ambapo juni mwaka huu jumla ya wasichana 41 kutoka wilaya za Ilemela na Nyamagan, mjini Mwanza walishiriki.

Wakati wa kilele cha mafunzo hayo jumla ya wasichana kumi walichaguliwa kusambaza elimu hiyo kwa wenzao wa mikoa ya Mara na Shinyanga, kumi wengine walipata nafasi ya kuudhuria mafunzo ya utayarishaji wa vipindi vya redio ambapo wanatazamiwa kurusha vipindi hivyo kwa kushirikiana na Afya Redio ya jijini Mwanza kwa nia ya kuielimisha jamii kuhusu haki zao.

Aidha washiriki wengine walitazamiwa kusambaza elimu waliyoipata katika mafunzo hayo katika klabu zao walizotoka na jamii inayowazunguka ili kutokomeza tatizo la mfumo dume kwa kuweka usawa katika ngazi za uongozi.

KIVULINI ni shirika linalojishughurisha na utetezi wa Haki za Wanawake na Haki za binadamu katika mikoa ya kanda ya Ziwa na Mkoa wa Singida.


MENEJA WA VIPINDI VYA AFYA RADIO, MR. FARAJA AKIFAFANUA JUU YA USHIRIKI WAO KATIKA KUANDAA VIPINDI VYA RADIO.
Meneja Utetezi na Sera wa Shirika la kutetea Haki za Wanawake KIVULINI, Bi. Celestina Nyenga akifundisha katika semina hiyo
BAADHI YA WASICHANA WAKIFUATILIA MAFUNZO HAYO.........

No comments:

Post a Comment