Monday, June 27, 2011

WANAWAKE TEGEMEZI HATARINI ZAIDI KUAMBUKIZWA UKIMWI.

Imeelezwa kuwa wanawake wanaopigwa au kutawaliwa kwa nguvu na waume zao wako hatarini zaidi kwa asilimia 48 kuambukizwa virusi vya UKIMWI kuliko wale walio katika  mahusiano yasiyo na ukatili.

Hayo yalibainishwa na meneja utetezi na sera kutoka Shirika la kutetea haki za wanawake KIVULINI, Bi. Celestina Nyenga wakati akitoa mada katika kamati ya kudhibiti UKIMWI ya halmashauri ya jiji la Mwanza (CMAC) juu ya Uhusiano kati ya UKIMWI na Ukatili dhidi ya Wanawake iliyokaa  Juni 17, 2011 katika ukumbi mdogo wa jiji.

Bi. Nyenga aliileza kamati hiyo kuwa kutokana na ukatili wa wanaume, wanawake hushindwa kuwashawishi hata kutumia kondomu na wao kukosa uamuzi wa kuvaa kondomu za kike jambo linalowaweka katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

Aliongeza kuwa utafiti uliofanywa na shirika hilo katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga na Singida waligundua kuwa wanawake wengi walio katika ndoa hubakwa na waume zao japo suala hilo huwa vigumu kuthilibitisha kisheria.

“ Ubakaji katika ndoa unafanyika kwa mwanaume kumwingilia mwanamke bila ridhaa yake…Mwanaume anaporudi usiku kutoka kwenye ulevi na kumkuta mkewe amelala huishia kumgongagonga kwenye kisigino kama ishara ya kumtaka kimapenzi na anapoona haamki mara nyingi umwingilia kwa nguvu” alieleza Bi. Nyenga.

Alisema kuwa ukatili wa kingono nchini Tanzania unafanyika kwa kiwango cha juu sana ambapo utafiti wa Garcia Moreno mwaka 2005 ulionyesha asilimia 40.4 ya wasichana walifanya tendo la kujamiiana kwa mara ya kwanza kwa kubakwa.

Akinukuu utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi(UNAIDS) alisema kuwa mwaka 2006, kati ya vijana watatu walioambukizwa virusi vya UKIMWI, wawili walikuwa ni jinsi ya kike.

Aliongeza kuwa wanawake wapatao milioni 13.2 sawa na asilimia 59 ya wanawake wan chi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanaishi na virusi vya UKIMWI ambapo vijana walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 wanye maambukizi, theluthi mbili ni wasichana.

Aidha alitaja tatizo la hali ya uchumi kuwa mojawapo ya sababu zinazomuweka mwanamke katika maambukizi zaidi ambapo wanawake na wasichana hulazimika kufanya ngono kwa hiari au kwa nguvu ili kupata chakula, pesa, ada ya shule au kupokea zawadi mbalimbali bila kujua kuwa zawadi hizo zitalipwa kwa tendo la kujamiiana.

Mbali na hayo, ukatili dhidi ya mwanamke uendelea punde anapogundulika kuambukizwa UKIMWI kwa kufukuzwa nyumbani na waume zao kwa sababu wao huwa wa kwanza kugundua hali hiyo wanapoudhuria kiliniki wakati wa ujauzito.

Aidha, Kivulini iliiomba kamati kuangalia jinsi ambavyo mipango yao ya maendeleo dhidi ya huduma za jamii, sera na miradi ya maendeleo inavyoweza kuhuisha suala la ukatili dhidi ya wanawake.

Akichangia katika mada hiyo, Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza, Mhe. Jacksoni Manyerere aiitaka jamii kutafuta mbinu za kuwafundisha watoto kusema hapana kwani yeye anaamini kuwa msichana hawezi kubakwa kama hataki.

Semina hiyo iliyoshirikisha wanakamati 25 wakiwemo watumishi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, wawaklishi wa madhehebu ya dini, madiwani na wawaklishi wa watu wanaoishi na virus vya UKIMWI ilikuwa na lengo la kutafuta namna ya kushirikiana ki-sera kuoanisha kasi ya maambukizi na ukatili wa wanawake.


Meneja Utetezi  na Sera, Shirika la kutetea haki za wanawake, Celestina Nyenga akitoa mada katika kamati ya kuratibu Ukimwi jiji la Mwanza(kulia kwake) ni Mwakilishi wa Wakristu katika kamati hiyo, Mchungaji Jacob Kituu.


Mwakishi wa Wanaume Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi jijini Mwanza, Bw. Chuu Waryoba akichangia mada.


Mwakilishi wa Wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi jijini Mwanza Bi. Zuhura Hussein akitoa mchango wake juu ya mada ‘Uhusiano kati ya Ukimwi na Ukatili dhidi ya Wanawake’ katika ukumbi mdogo wa jiji.

Mtahiki Meya wa jiji la Mwanza, Mhe. Jackson Manyerere akitoa mchango wake kuhusu uhusiano kati ya Ukimwi na Ukatili dhidi ya Wanawake(kulia kwake) ni Naibu Meya wa jiji hilo(Bw………) na Mratibu wa Ukimwi katika halmashauri ya jiji la Mwanza Bw. Damas Mukama.

No comments:

Post a Comment