Thursday, June 23, 2011

FAHAMU JINSI ANGELA NA ANGELINA WALIVYOFANIKISHA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA WAFANYAKAZI WA NDANI-ILO.



Angela (kushoto) na Angelina wakipozi eneo la KIVULINI,mjini Mwanza baada ya kutoka Uswizi.

INAAMINIKA kuwa katika maisha mlango mmoja wa mafanikio unapofungwa basi mlango mwingine huwa umefunguliwa na ambapo mtu uhisi mafanikio yapo maili 100 huenda inchi moja tu huwa imesalia.

Hayo yalidhihirishwa na wawakilishi wa Tanzania katika mkutano wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) mjini Geniva-Uswizi, Angela Benedicto(24) na Angelina Nyamuhanga(17) ambao awali walikwisha kata tamaa ya mafanikio katika maisha kutokana na hali halisi ya maisha wanayoshi.
[+/-] show/hide this post
Wasichana/watoto hao kutoka Mwanza na Musoma ambao ni wafanyakazi wa kazi za nyumbani waliiwakilisha Tanzania katika mkutano wa kimataifa ulioanza mwezi Mei na kumalizika Juni 2011 mjini Geniva kwa kutanguliwa na ujumbe kutoka kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Mkutano huo ambao ni  wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ulianza ‘rasmi’ Juni Mosi baada ya kutanguliwa na mkutano wa wadau kupanga hoja mjini Geneva, Uswisi ambapo Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi saba duniani ambao walikuwa wageni maalumu na kupangwa kuhutubia siku ya kilele chake Juni 16.

Tofauti na miaka mingine ambayo wafanyakazi wa nyumbani Tanzania walituma uwakilishi wa maandishi, mwaka huu wajumbe kamili walihudhuria mkutano huo kabla ya kuanza rasmi kwa wageni maalum (wakuu wan chi).

Katika mkutano huo ulioudhuriwa na wajumbe wa mabaraza ya kazi kutoka nchi mbalimbali duniani, wawakilishi kutoka Tanzania na wenzao kutoka nchi nchi za Ufilipino na Costa-Rica pamoja na kuelezea mazingira ya kazi zao walikuwa na jukumu la kupigia debe kifungu cha nne(4),kipengele cha nne(4) cha mkataba wa ajira duniani kuhusu elimu na mazingira bora ya kazi kabla ya mkutano huo kuanza rasmi.

Pamoja na kujadili kipengele hicho, wawakilishi hao walitakiwa kuwashawishi wajumbe wa mkutano huo kukipitisha na kujadili kwa pamoja juu ya umri wa wafanyakazi wa nyumbani, usalama wa afya zao kazini, elimu na namna ya kuwajengea uwezo wa kufikia maisha bora.

Aidha washiriki walitakiwa kutoa maoni yao dhidi ya aina ya kazi zinazotakiwa kufanywa na wafanyakazi wa nyumbani, mazingira na hali halisi wanamofanyia kazi, mazingira yanayohatarisha afya zao, uslama na makuzi ya mtoto anayefanyakazi za ndani na kutakiwa kwa pamoja kupinga ajira kwa watoto.

Mbali na hayo, kipengele hicho kinakataza kufanyakazi usiku, ukomo wa masaa ya kazi kwa kutoa fursa kwa mfanyakazi wa ndani kupumzika, kuwasiliana na familia zao pamoja na fursa ya kujiburudisha. Pia walitakiwa kuweka taratibu za kufuatilia mazingira ya kazi zao na mikataba yao ya kazi.

Wawakilishi hao wanasema kuwa ziara hiyo imefufua upya matumaini yao na watoto wenzao ambao hapo kabla hawakutegemea mchango wa kazi zao kutambuliwa na kuthaminiwa kimataifa.

“ Kutokana na kunyanyaswa na kudharauliwa kwa kazi zetu za (ndani) nyumbani, hatukutegemea kama ipo siku ambayo tunaweza kupanda ‘madege’ makubwa kuiwakilisha nchi huko Ulaya na kukutana na viongozi wakubwa ambao kabla tuliwaona na kuwasikia tu kwenye vyombo vya habari” Wanaeleza.

Waliongeza kwamba tofauti na mawazo yao kuwa safari kama hizo huwa ni za viongozi wachache, familia bora na watu wenye kisomo, ziara hiyo imefufua fikira mpya na nuru ya mafanikio kwa wafanyakazi wa majumbani kwa kuona mchango wa kazi zao umetambuliwa kimataifa.

Swali ambalo wengi wanajiuliza ni kuwa waliwezaje basi wafanyakazi wa nyumbani kuwakilisha nchi kimataifa?

Kujibu swali hilo, Angela na Angelina hawasiti kulitaja Shirila la kutetea haki za wanawake KIVULINI la jijini Mwanza kwa kuwaibua, kuwajengea uwezo na thamani katika jamii ya watanzania hadi kupata nafasi hiyo.

KIVULINI kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kwa muda murefu wamefanya jitihada za kuwatambua wanawake wanaofanya kazi hatarishi, kuwakusanya kwenye vikundi na kuwapa semina za mara kwa mara kwa mikoa ya kanda ya Ziwa hadi kutuma wawikilishi hao katika mkutano wa shirika la kazi duniani.

Wakieleza ukubwa wa tatizo, Angela na Angelina wanasema kuwa pamoja na nchi nyingi kuwa na wafanyakazi wa nyumbani wanaofanyakazi katika mazingira hatarishi katika umri mdogo,ni nchi tatu tu za Tanzania, Costa-Rica (wawakilishi wawili wawili) na Ufilipino iliyokuwa na mwakilishi mmoja.

Ni uzoefu gani wameupata kutoka kwa wenzao katika mkutano huo?
Angela na Angelina wamasema kuwa tofauti na hapa kwetu Tanzania, wafanyakazi wa ndani katika nchi za Costa-Rica na Ufilipino hupata fursa za elimu ambapo nyakati za asubuhi hufanya kazi za waajiri wao na jioni huudhuria vipindi darasani.

Wanaongeza kuwa serikali na jamii katika nchi zao huthamini dhamana wanayokuwa nayo wafanyakazi wa nyumbani katika kulea watoto wa waajiri wao,kutunza nyumba na kupokea wageni hivyo kuona umuhimu wa kuwaelimisha wafanyakazi wao.

Angela na Angelina ni akina nani hasa? Na ni kwanini wachaguliwe wao kuwakilisha nchi?
 Kwa pamoja wanakili kutokuwa na elimu ya kutosha ya darasani wala vipaji vingine zaidi ya karama waliyopewa na mwenyezi Mungu ya kujieleza kwa ufasaha mbele za watu na ujasiri wa kueleza matatizo yao ya kazi bila woga.

Wote wanataja sababu ya kujiingiza katika kazi hiyo kuwa ni kutokana na adha ya kuyumba kwa familia na ndoa za wazazi wao na hatimaye  kuvunjika wakingali wadogo hivyo kulazimika kubeba majukumu mazito ya kulea familia katika umri huo.

Aidha tofauti na Angelina ambaye hakubahatika kusoma hata darasa moja, Angela  baada ya kufeli mtihani wa kidato cha nne na kukutana na ukali wa baba na mama yake wa kambo alilazimika kujitafutia ajira bila mafanikio na hatimaye kumpata mwajiri wa kazi za nyumbani mwenye moyo wa kumwendeleza kielimu.

Angelina anasema kuwa hakubahatika kuonja hata darasa moja kutokana na kifo cha baba yake aliyemuacha na miaka miwili.

“Maisha yalianza kuwa magumu baada ya baba kufariki mwaka 1996 kwa ugonjwa wa ini yeye akiwa na mimi nikiwa umri wa miaka miwili tu kwani pamoja na kuwa mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) hakufanikiwa kujengea hata nyumba ya kuishi zaidi ya kibanda cha majani kijijini” Anaeleza Angelina.

 Anasema  maisha yalikuwa magumu sana kijijini ambapo mama yao baada ya kurubuniwa na mwanaume aliamua kuuza shamba la urithi kwa shilingi 20,000 na kuhamia mjini Bukoba mkoa wa Kagera sambaba na kaka yake na dada ambao kwa hivi sasa wanaishi na baba yao mdogo kijijini kwa babu.

Akielezea safari yake ya kazi za nyumbani, Angelina anasema kuwa ilianza akiwa na miaka  kumi baada ya baba yake wa kufikia kuachishwa kazi misheni na baadaye kuwatelekeza kwa kuhamia kwa mke mwingine ambaye alimuoa huko na kuwaacha wasijue pa kwenda.

Anasema kuwa baada ya kuchangiwa nauli kidogo na Misheni alipofanya kazi babayao wa kambo na hela kidogo aliyopata kaka yao ambaye kwa wakati huo alifanya vibarua bandarini waliweza kurudi Musoma na kupanga chumba kwa shilingi 3,000 mwaka 2004 hivyo yeye kulazimika kutafuta kazi za ndani kuendesha familia.

Kwa mshahara wa shilingi 20,000 Angelina anaweza kulipia chumba alichopanga mama yake, maji na matumizi ya nyumbani pamoja na matumizi yake binafsi. Pia kwa mshahara huo huo huwasaidia dada yake(mama wa watoto watatu) na kaka yake ambaye ni fundi baiskeli kijijini Tarime

Aidha pamoja na changamoto wanazokutana nazo Angela na Angelina wanataja faida ya kazi za nyumbani kuwa imewapa uwezo wa kujifunza mambo mengi ya kifamilia kama vile kulea watoto, kutunza nyumba, kupokea wageni na mambo mengine ambayo hata umri wao unakuwa bado kama jinsi ya kuishi na mme vizuri katika ndoa kwa kugundua makosa ambayo mara nyingi huwafarakanisha wanaume na wake zao.

Nini faida ya safari yao Uswizi?
Wanasema baada ya safari hiyo ambayo iliwafunulia mambo mengi sasa wanaweka mkakati wa kuhakikisha wafanyakazi wenzao wa nyumbani wanathaminiwa na kupata haki kama wafanyakazi wengine na kudai haki ya elimu.

Wanataja mbinu watazozitumia kuwa ni pamoja na kuwatembelea majumbani mwao na katika vikundi mbalimbali vilivyokwisha kuanzishwa kwa kushirikiana na Shirika la kutetea haki zao la KIVULINI.

Aidha wanatoa wito kwa waajiri kuwachukulia wafanyakazi wao kama sehemu ya familia kwa kuthamini utu na haki zao za msingi kama binadamu wengine na jamii kuvunja ukimya kuhusu matendo maovu wanayofanyiwa wafanyakazi wa nyumbani.

Pia waliiomba serikali kuweka vipaumbele katika mikataba na sheria mbalimbali ilizokwisha zisaini kuhusu ajira kwa watoto na haki za binadamu badala ya kuishia kwenye makabrasha!

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisisitiza kuwa… kulingana na viwango vya ILO, mfanyakazi wa ndani hana tofauti na wengine wanaopaswa kufanya kazi zisizo za kushurutishwa.

“Mkataba ukisharidhiwa kwa ajili ya wafanyakazi wa ndani, tutauchukua na kuupeleka bungeni ili ujadiliwe na ukipitishwa. Ina maana Sheria iliyopo itaongezewa nguvu” alisema Waziri Kabaka.

Akifafanua kazi za staha kama zilivyoainishwa na mkutano huo kuwa ni pamoja na kuwekewa akiba katika mifuko ya hifadhi ya jamii, kupata haki na uhusiano wa mazungumzo kati ya mwajiri na mwajiriwa.

"Mwajiri atalazimika kumchangia kwenye hifadhi ya jamii na sisi tutahakikisha tunasimamia na kufuatilia hawa watumishi wa ndani watendewe haki," alisema.

Alifafanua kwamba, wameiomba ILO iwezeshe kufanya ukaguzi majumbani kubaini kama wafanyakazi hao wanatimiziwa haki zao.

Ukaguzi huo utalenga kubaini waajiri wasiowalipa wafanyakazi kwa kuzingatia kima kilichotangazwa ambacho mfanyakazi wa ndani anayeishi katika nyumba husika anapaswa kulipwa kuanzia Sh 20,000, asiyeishi nyumbani ni Sh 65,000 na wanaofanya kazi kwa mabalozi na viongozi ni Sh 80,000.

Mbali na Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mkuu wa nchi pekee aliyealikwa kutoka barani Afrika, wageni maalumu wengine walikuwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Susilo Yudhoyono na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Viongozi wengine waliohutubia mkutano huo uliojumuisha washiriki kutoka nchi zote 183 wanachama wa ILO ni Waziri Mkuu wa Russia, Vladimir Putin; Rais wa Jamhuri ya Uswisi, Micheline Calmy-Rey; Rais wa Finland, Tarja Halonen na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestine, Salam Fayyad.

Kadharika mkutano huo wa 100 tangu kuanzishwa kwa ILO mwaka 1919, ulihudhuriwa na jumla ya watu 7,000 na kushirikisha viongozi wa nchi na serikali wa zamani, mawaziri wa nchi mbalimbali, taasisi za kimataifa, na taasisi za kiraia.
Mada za jumla zilizozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira duniani, zahama ya kimataifa ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, jinsi ya kuongeza kiwango cha kulinda watu zaidi duniani kupitia mifuko ya hifadhi za kijamii, na haki za wafanyakazi na watumishi kazini na hasa zile za watumishi wa ndani.


SAFARI YA USWIZI KATIKA PICHA.
 
...wakipata mawidha kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa KIVULINI, Bi. Maimuna Kanyamala (hayupo pichani) kushoto ni mlezi wao katika safari hiyo Bi. Groly

Safari sasa imeiva........wanaelekea uwanja wa ndege wa Mwanza kukwea pipa.


Angela akisimulia jinsi safari yao ilivyokuwa katika hafla fupi ya kuwapongeza iliyofanyika katika eneo la bwawa la kuogelea KIVULINI-Mwanza. 
      ACHA NIJICHANE MWENZANGU...USWIZ SI MCHEZO.
Baadhi ya wadau wakiburudika katika hafla hiyo.

YAANI HATA MIMI WAMENIPIGA BAO..........................................................................................................! 
 
Diwani wa kata ya Isamilo naye alikuwepo...

No comments:

Post a Comment